WADAU WA ZAO LA MWANI WAKUTANA KATIKA JUKWAA MOJA

Shirika la LANGO kwa ufadhili wa shirika la OXFAM Tanzania limeandaa jukwaa  lililowakutanisha wadau mbalimbali wa zao la mwani ikiwemo wakulima, makampuni yawanunuzi, pamoja na Watendaji wa serikali ambao ni Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa, Afisa Ushirika Manispaa, Afisa Uvuvi na Maliasili Tarafa, Watendaji ngazi ya Kata na Mitaa kutoka kata ya Mchinga Manispaa ya Lindi katika kujadili hali ya masoko katika zao hilo, changamoto na namna wadau hao wanavyoweza kuchangia kukua na kuwanaufaisha wakulima wa zao hilo.

Wakulima hao kutoka kata ya Mchinga wametoa kilio chao cha muda mrefu cha bei duni ya mwani mdogo ya Shilingi 400/= ukilinganisha na bei inayotumika Zanzibar ambayo ni Shilingi 1,000/= ingali mnunuzi anayuenunua Zanzibar ndiye yule yule anayenunua na Mchinga.

Akijibu hoja hiyo, Bw. Mohammed Mikidadi  ambaye aliwakilisha kampuni ya REDO BIASHARA LTD inayonunua mwani katika Kata ya Mchinga amesema jambo kubwa linaloleta utofauti wa bei ya mwani kati ya Mchinga na Zanzibar ni masharti magumu yaliyowekwa na seikali ya Tanzania Bara  yanayoongeza gharama za usafrishaji wa zao hilo. Pia aliongeza kuwa kwa upande wa Tanzania Bara kuna mchakato mgumu na ghali wa kupata leseni ya ununuzi wa mwani jambo linalowapeleka hata wao kununua zao hilo kwa bei ya chini.

Bi. Judith Jaccob, Afisa Ushirika kutoka Manispaa ya Lindi akizungumza kwa upande wa serikali amewataka wakulima hao  kusimamia msimamo wao wa kuanzisha Ushirika ambao utaweza kuwapa nguvu na sauti moja kwenye  kupanga bei ya mwani. Amesema kuwa ni ngumu kwa kipindi hiki kwa wakulima kupanga bei yenye msimamo ingali kila mkulima anasimamia bei yake binafsi.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Lindi Bw. Methusela Magayane amewataka wakulima hao kuboresha kilimo hiko ili mazao yawe mengi yenye uhakika, na yaliyo bora ili hata wanunuzi wasifikirie mara mbili mbili kununua mwani kwa wakulima hao kwa bei nzuri. Amewataka wakulima hao kutumia vikundi vyao kwenda ofisi za Maendeleo ya Jamii Manispaa kuomba mikopo itakayowawezesha kuboresha kilimo hiko.Leave a Reply