WANANCHI KUJENGEWA UWEZO WA KUWEZA KUTAMBUA, KUCHAMBUA NA KUTATUA CHANGAMOTO ZAO WENYEWE

Shirika la LANGO kwa kushirikiana na shirika la TWAWEZA East Africa limefanya mkutano na viongozi wa halmashauli ya Mtama, na viongozi wa vijiji vya Halmashauri ya Mtama kutambulisha programu mpya ya Uraghbishi inayotarajiwa kutekelezwa hivi punde katika Halmashauri hiyo.

Akiongea katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la LANGO Bw. Michael Mwanga ameeleza kuwa programu hiyo inatarajiwa kutekelezwa katika vijiji kumi (10) vya Halmashauri ya Mtama ambavyo ni; Namangare, Nahukahuka, Chihuta, Sudi, Mmumbu, Hingawari, Mwangu, Mtakuja, Mandwa, na Mtualonga.

Wananchi katika vijiji hivi watapatiwa mafunzo ya dhana ya uraghbishi ambayo itawapa uwezo wa kujitambua na kuelewa nafasi yao kwamba wao wenyewe ndiyo wahusika wakuu katika kuibua, kuchambua na kutatua changamoto zilizopo katika jamii zao wenyewe.

Kwa upande wake Bw. Richard Temu ambaye ni Afisa Mwadamizi Idara ya Ushiriki kutoka shirika la TWAWEZA  aliongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa sana kwa wananchi kubadili fikra zao, kwamba kuachana na nadharia ya kusubiri maendeleo yaletwe na watu wengine badala yake wanajamii wenyewe wahusike katika kila ngazi ya maendeleo; waone kwamba wanaweza kuwa watendaji wakuu wa maendeleo katika jamii zao.

Temu aliongeza kwamba ni kweli siri ya mtungi aijuaye kata; lakini maji ambayo yanaishi ndani ya mtungi yapo kwenye nafasi nzuri zaidi ya kutambua hali halisi ya mtungi kuliko kata ambayo huingia na kutoka ndani ya mtungi kwa msimu tu. Hivyo wanajamii wanatakiwa kujihusisha kufanya kazi katika ngazi ya jamii, pamoja na jamii, kwa ajili ya wanajamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la LANGO Bw. Michael Mwanga akieleza jambo wakati wa mkutano huo

 

Richard Temu, Afisa Mwandamizi idara ya Ushiriki kutoka shirika la TWAWEZA East Africa akitoa wasilisho katika mkutano huo

Viongozi wa serikali za vijiji wakifuatilia mjadala kwa makini
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mtama Bw. Wenstelaus Mbilango akitoa neno la ufunguzi katika mkutano huoLeave a Reply