USIMAMIZI MZURI WA MAPATO YATOKANAYO NA SEKTA YA UZIDUAJI NDIO MHIMILI MUHIMU WA MAENDELEO YA JAMII ZETU

Hayo yamezungumzwa katika warsha ya kubadilishana uzoefu, kujadili mafanikio na changamoto juu ya usimamizi wa gawio la 20% ya Tozo ya Huduma kutoka halmashauri ya Kilwa itokanayo na sekta ya Uziduaji wa Gesi asilia, iliyoandaliwa na shirika la LANGO kwa ufadhili wa wa shirika la Oxfam iliyokutanisha viongozi wa kijiji waliopo madarakani, waliopita pamoja na Waraghibishi kutoka katika kata ya Songosongo Wilayani Kilwa.

“Lengo kubwa la warsha hii ni kukutanisha wadau wa maendeleo ya hiiki kijiji cha Songosongo ili kujenga uelewa wa pamoja baina ya viongozi wanaoendelea, viongozi waliopita na waraghibishi juu ya jitihada zao wanazofanya katika kufuatilia kiasi kinachoingia hapa kijijini kutoka halmashauri ya wilaya ya Kilwa ili tuwe na uelewa wa pamoja na kuweka mikakati thabiti ya kuleta maendeleo yenye tija. Tunachotaka songosongo kuwe na maendeleo, na maendeleo hayaletwi na mtu mmoja na ndio maana ya kuwakutanisha hapa ninyi wadau wa maendeleo. Usimamizi mzuri wa mapato yatokanayo kwenye sekta ya uziduaji ndio mhimili muhimu wa maendeleo ya jamii zetu” Mkurugenzi wa Shirika la Lango Bw. Michael Mwanga.

Kwa upande wake Mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Songosongo Bw. Mzee A Mjaka alieleza “Kwa uzoefu nilioupata, inahitaji umakini mkubwa sana wa kushughuika na hii sekta ya uziduaji. Kwanza kama mweyekiti wa kijiji ni lazima uwe na taarifa za kina juu ya makampuni yote yaliyowekeza katika kijiji chako. Lazima ufahamu idadi yake na wamiliki wake maana kuna tabia ya hizi kampuni kubebana ili kukwepa kodi kiholela.”

Aidha, Bw.Mjaka akaongeza kwamba kama viongozi lazima wawe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba miradi inayofanywa na haya makampuni yanalenga hasa vipaumbele vya kijiji mana haya makampuni huwa na ujanja wao wa miradi wanayoitaka wao ili kuwepa gharama.

“Vile vile viongozi tukwepe kuingia makubaliano yasiyo ya maandishi baina ya wawekezaji kuepusha migogoro isiyo ya lazima. Haya makampuni yanapokuja huwa wanakua na lugha nzuri na ahadi za kulaghai wakiahidi kuisaidia jamii hisika lakini baadae wanageuka. Lakini ahadi hizo zikiwekwa kwenye maandishi inaipa jamii nguvu ya kudai kisheria Zaidi.

Hii kampuni ya TPDC walivyokuja kuanza kazi waliahidi kutoa ajira kwa wanawake na wanaume, lakini pia wangesambaza maji, kuleta boti ya wagonjwa, wangejenga soko pamoja na ofisiya kijiji. Lakini kwa tabu sana walifanikiwa kuleta boti ya wagonjwa ambayo haina viwango, na maji ambayo waliyaleta kwa kuyadai sana tena wakayaweka sehem moja tu badala ya kuyasambaza.

Jambo linguine linalotupa tabu ni mikataba ya hawa wawekezaji kufungwa fungwa. Lazima kama wananchi tujue kwamba utendaji na uhisani wa hawa wawekezaji kisheria unaanzia wapi na kuishia wapi na mikataba hiyo ipatikane kwa wakati stahiki hata pale tunapoenda kwenye ofisi za wakurugenzi wa halmashauri za wilaya tuipate” Mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Songosongo Bw. Mzee A Mjaka.

Katibu wa Waraghibishi wa kata ya Songosongo Bw. Kassim Jaka kwa upande wake akaeleza “Sisi ni waraghibishi, kwa maana nyingine ni mawakala wa mabadiliko katika jamii. Kazi yetu ni kuibua hoja ambazo tunaamini zinaweza kuchochea maendeleo ya jamii yetu na sio waleta vurugu kama ambavyo wengine wanadhania. Kwahiyo hata katika sekta ya uziduaji tumekua tukifuatilia kwa ukaribu sana kuhusu usimamizi wa 20% ya Tozo ya Huduma ambayo kama kijiji cha Songosongo tunapaswa tuipate kutoka katika halmashauri ya wilaya ya Kilwa ambayo wao wanaipata kaika sekta ya uziduaji. Changamoto tunayoipitia ni kuonekana kama vile sisi tunahamasisha vurugu lakini sivyo, sisi tunaibua hoja kwa njia ya amani kabisa pasi kuvunja sheria za nchi. Sisi ni wachochezi wa maendeleo na hatujafungamana na itikadi yoyote ya kisiasa wala kidini. Kwa hiyo tunaomba serikali itupe ushirikiano pale tunapohitaji taarifa au takwimu za miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yetu”.

“Mwenyekiti wa Kijiji Cha Songosongo Bw. Swaliya Hassan Said akaongeza kia warsha hii imekua ni ufunguo kwake kwani imempa picha kubwa zaidi juu ya suala la Tozo ya Huduma kutoka katika sekta ya Uziduaji. Uzoefu alioupata kutoa kwa mwenyekiti mstaafu umempa uelewa mpana zaidi ambao atautumia ili kuhakikisha Songosongo inaendelea.”

 

 

Afisa Mradi wa shirika la LANGO Bi. Aina Pero akitoa wasilisho katika warsha hiyo
Mkurugenzi wa shirika la LANGO Be. Michael Mwanga akitoa hoja katika warsha hiyo
Wanajamii wa Songosongo wakifuatilia mjadala Kwa makini
Katibu wa waraghibishi Kijiji Cha Songosongo Be.Kassim Kaka akitoa wasilisho Kwa niaba ya waraghibishi”.

Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji Cha Songosongo Bw. Mzee A Mjaka akichangia hoja katika warsha hiyoLeave a Reply