VIKUNDI VYA WAKULIMA WA MWANI MCHINGA KUUNDA USHIRIKA

Maamuzi hayo  ya kuunda ushirika wa Mwani kata ya Mchinga yameafikiwa katika kikao kilichowakutanisha vikundi vya zamani na vikundi vipya vya wakulima wa mwani katika kata ya Mchinga Manispaa ya Lindi, kikao kililenga kubadilishana uzoefu, mafanikio, changamoto na fursa walizozipata katika vikundi hivyo ili kuboresha na kuongeza uzalishaji wa zao la mwani.

Vikundi hivyo vimefikia uamuzi huo baada ya kuona faida za vyama mbalimbali vya ushirika  vya wakulima wa mazao mengine kama korosho na ufuta, jinsi  ushirika unavyotumika kama,  miamvuli ya kuwatambulisha wakulima pamoja na kuwasogeza kwa pamoja kupata fursa mbalimbali katika kilimo.

Wameongeza  kuwa ziara ya Zanzibar iliwapa chachu na ari, kwa kuona jinsi ushirika wa Furahia Wanawake Cooperative ulivyo wanufaisha wakulima wa mwani Paje, Zanzibar ikiwemo kuivutia serikali kuwapa vitendea kazi vinavyorahisisha shughuli za kikundi hiko.

Kwa sasa wanavikundi hao wa Mchinga wapo katika michakato ya awali ya kuanzisha ushir ika huo ikiwemo kuchangishana ada na wanatarajia kuanzisha ushirika huo mapema mwezi Agosti mwaka huu.

Shirika la LANGO kwa udhamini wa shirika la Oxfam Tanzania limeratibu vikao hivyo kwa lengo la kuibua mijadala baina ya wakulima wa zao la mwani ili waweze kupanua uelewa na kuongeza uzoefu ili wana Mchinga wafanye kilimo cha mwani chenye kuleta tija.



Leave a Reply