SERIKALI YA LINDI KUWEKA MIKAKATI THABITI JUU YA UJIO WA MRADI WA GESI WA LGN

Meya wa Lindi, Frank Magari amesema serikali mkoani humo imeazimia kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika fursa za uwekezaji zitakazoambata na ujio wa mradi mkubwa wa kuchakata gesi asilia wa LNG unaotarajia kuanza hivi punde katika Kata ya Mbanja  Manispaa ya Lindi.

Magari amezungumza hayo katika jukwaa la uziduaji  lililoandaliwa na shirika la LANGO kwa ufadhili wa shirika la OXFAM, jukwaa lililokutanisha wadau wa sekta ya uziduaji kutoka wialaya ya Lindi, Ruangwa na Kilwa.

Aidha, ametanabahisha kwamba serikali hiyo imeshaanza kupeleka huduma za kijamii katika kata ya Mbanja ikiwemo ujenzi wa hospitali kubwa kulingana na mahitaji ya huduma za afya yatakayojitokeza punde baada ya mradi huo kuanza.

Katika jukwaa hilo, Mchumi wa Manispaa hiyo, Julius Ndele alisema kwa upande wao wameendelea na maandalizi na wamekuwa tayari kujifunza kutoka kwa wenzao wa Kilwa na Ruangwa ambao tayari wana miradi ya uziduaji wanayoisimamia.

Alisema kazi ya kwanza waliyoifanya katika kujiandaa na mradi huo ni kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi, kulipa fidia kwa wakazi wa eneo la mradi, kuweka huduma za miundombinu rafiki kuelekea kwenye eneo la mradi na kuendelea kuelimisha wananchi kupitia redio na televisheni kuhusu fursa zitakazojitokeza katika mradi huo,.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza la Mashehe Mkoa wa Lindi, Shehe Said Mohammed amewataka wananchi wa Lindi kuwa tayari kujiandaa na mabadiliko ya kijamii kutokana na ujio wa mradi huo.  “Tuna mfano hapa wa ujenzi wa barabara. Maisha yalibadilika ghafla, vyumba vilikuwa ghali, chakula ghali, na hapo walikuwa watu 1,000 tu walioingia Lindi kwa kazi hiyo,hivyo kwa mradi huu wa gesi utakaoingiza watu zaidi ya 10,000 mambo yatakuwa mengi zaidi hivyo hatuna budi kujiandaa,” Alisema Shehe huyo.

Akaongezea kuwa wananchi wa Lindi wanaweza kubaki kuwa wasindikizaji kama hawatakuwa wamejiandaa kutumia fursa hizo na pia watabaki kuwa na maisha duni kama watakuwa wamejiaandaa kinyume.

Katika jukwaa hilo, Mkurugenzi wa LANGO Ndg. Michael Mwanga ameeleza kuwa wameandaa jukwaa hilo ili kuwapa fursa wadau kujadili masuala yahusuyo sekta ya uziduaji katika mkoa huo, kubadilishana uzoefu na changamoto ili kuhakikisha usimamizi na utekelezaji wa rasilimali hizi zinaleta tija inayokusudiwa kwa wakazi wa Lindi.

 

 Leave a Reply