Wakazi wa mkoa wa Lindi hususani wanaokaa kuzunguka mradi wa kuchakata gesi wa LNG, uliopo katika kata ya Mbaja katika Manispaa ya Lindi wapewa onyo kuepuka matapeli wanaochangisha wananchi hao fedha kwa kuwaahidi kuwapatia nafasi za ajira pindi mradi huo utakapoanza.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Shirika lisislo la Kiserikali la LindiĀ (LANGO) Ndg. Michael Mwanga wakati wa kikao kazi kilichoitishwa na shirika hilo na kuhusisha wadau kutoka sekta mbalimbali ikiwemo serikali ya Mkoa.
Aliwataka wadau wanaohusika na taarifa za mradi huo kuhakikisha kwamba wanatoa taarifa kwa wananchi kwa weledi ili kuepuka mkanganyiko wa taarifa.
Kikao kazi hicho kilichoshirikisha watu 26 ikiwemo Mbunge wa Lindi, Meya wa Manispaa ya Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, na Diwani wa Kata ya Mbanje kilikua kinaangalia mahali ambapo mradi utatekelezwa.
Hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea Mkoa wa Lindi aliwataka wananchi kuendelea kujiandaa na mradi huo mkubwa kwa kuweka mazingira sawa ya utoaji huduma kwani watu wengi wataishi Lindi wakitekeleza mradi huo.
Majaliwa alisema kwamba serikali inaendelea na mikakati yake ya kuhakikisha kwamba mradi huo utakao ajiri watu zaidi ya 20,000 unafanikiwa.