Shirika la LANGO kwa ufadhili wa shirika la OXFAM International limefanya ziara ya mafunzo jijini Tanga kwenye mradi wa bomba la mafuta la EACOP. Ziara hiyo imeshirikisha wadau wa mradi wa kuchakata gesi asilia wa LNG (Lindi) ambao ni shirika la LANGO, viongozi wa Manispaa ya Lindi akiwemo Mchumi wa Manispaa ya Lindi, viongozi wa serikali za kata ya Mbanja pamoja viongozi wa serikali za mtaa wa Likong’o ambako mradi wa LNG unajengwa. Lengo kubwa likiwa ni kujifunza na kubadilishana uzoefu juu ya utekelezwaji wa sera za Uwezeshwaji Wazawa (Local Content Policy) na Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR) katika maeneo ya utekelezwaji wa miradi hii mikubwa.
Katika majadiliano wadau wamezidi kusisitiza wananchi kuchukua hatua za dhahiri za kujiandaa kukamata fursa zinazoambatana na miradi hii ili waweze kunufaika nayokama anavyoeleza Afisa Maendeleo wa Jiji la Tanga Bw. Moses Kisibo “Ukiachana na vikundi ambavyo vimehamasishwa kujiunga ili kuunganisha nguvu ya pamoja katika kutambua na kuzichangamkia fursa za miradi hii mikubwa, lakini sisi kama halmashauri tunashirikiana na idara mbalimbali za halmashauri kutoa hamasa kwa jamii kuendelea kutazama mradi huu wa bomba la mafuta la EACOP kama fursa ambayo itawaondoa wananchi katika hali ya kipato duni kwenda kwenye kipato bora. Sisi kama idara ya maendeleo ya jamii tunakua kama chachu ya kuifanya jamii ibadilike, na ndio maana tumewashauri vijana kuingia katika biashara ya mfumo wa kidigitali ili waweze kuendana na ulimwengu wa sasa wa kiteknolojia”.
Mkurugenzi wa shirika la LANGO pia akasisitizia kua wananchi wanatakiwa kuangalia ni maeneo gani ya biashara na huduma wanazotoa zinatakiwa kuboreshwa ili kuendana na mahitaji ya wageni. Mfano wenye nyumba za wageni warekebishe au wajenge nyumba zenye viwango, wamama ntilie na wenye migahawa waboreshe migahawa na chakula chao, kama wafugaji wafuge kuku wenye viwango watakaouzika sokoni. Tuhakikishe huu mradi unabadilisha kipato cha mtu mmoja mmoja kuanzia ngazi ya kaya.
Aidha Mchumi wa Manispaa ya Lindi Bw. Julius Ndere ametoa angalizo kwa wananchi wanauza ardhi zao kiholela ili kupata fedha za haraka “Mimi natoa angalizo kwa wananchi kutunza na kulinda ardhi zao. Hii miradi mikubwa inafanya uhitaji wa ardhi kuwa mkubwa, kwahiyo watu wasishawishike sana kuuza ardhi zao wakati huu kwa bei ya tamaa wakati ardhi hizo wangezitunza zingeweza kuwaletea faida kubwa siku za mbeleni. Tuangalie tusije kuwa wageni katika nchi yetu wenyewe”.
Lakini pia wananchi wameshauriwa kuwa waangalifu dhidi ya maambukizi ya magonjwa hatarishi hususani virusi vya UKIMWI pamoja na mimba za utotoni. Wameshauriwa kila kaya itoe elimu jamii kwa vijana wao juu ya matokeo hasi ya miradi hii ambayo mara nyingi inaleta mwingiliano mkubwa wa wageni katika maeneo yao. Imeshauriwa kuwahimiza vijana na watoto kuendelea kushikilia masomo yao na sio kuhadaika kuacha masomo na kukimbilia ajira za muda mfupi kwenye maeneo ya miradi.
Halmashauri zimeshauriwa kufanya tathmini ya makundi ya vijana waliopo kwenye maeneo ya mradi kuona kama wana ujuzi na sifa za kuajirika ili fursa hizo zisichukuliwe na wageni. Kuwaandaa kwa kuwaongezea ujuzi katika vitu ambavyo wanaweza kuvifanya. Na maandalizi hayo yanatakiwa kufanyika mapema kabla mradi haujaanza kwani mradi hauwezi kusimama ukisubiria wananchi wajiandae, lazima watukute tuko tayari.